Mwalimu adaiwa kumlewesha mhitimu wa darasa la saba na kumbaka shuleni

0
44

Mwalimu wa taaluma katika shule ya Msingi Rulanda, wilayani Muleba, mkoani Kagera anatuhumiwa kumpaka vitu vinavyodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya kisha kumbaka mhitimu wa darasa la saba aliyefika shuleni kufuatilia matokeo yake.

Binti huyo (13), amedai kuwa alikwenda shuleni hapo Oktoba 30, mwaka huu saa tisa alasiri na kukutana na mwalimu huyo ambaye alimweleza kuwa amepata Daraja D, na baada ya kupewa matokeo, mwalimu huyo alimtaka arudi shuleni hapo saa 10 jioni ili ampatie ushauri kutokana na kupata matokeo yasiyoridhisha.

Msichana huyo amedai baada ya kuitikia wito kwenye moja ya madarasa alikokuwa anasoma, mwalimu huyo alifika na kufunga mlango na madirisha na kumtaka avue nguo, ambapo ameeleza kuwa alimpaka vitu sehemu mbalimbali za mwili kisha akapoteza fahamu, na alipozinduka alimwona akimchungulia dirishani na kumtaka aondoke.

Mama wa mtoto huyo (jina limehifadhiwa) ameeleza kuwa mwanaye alifika nyumbani saa 1:30 jioni, alipomhoji alidai kuwa mwalimu wake alimfungia ndani na kumziba mdomo asipige kelele na kumpaka dawa. Amedai alipomchunguza alibaini alikuwa ameingiliwa kutokana na michubuko sehemu za siri.

Baba amuua mtoto wake baada ya kugombana na mke wake

“Tulikwenda kituo cha Polisi tukapewa PF3 kwa ajili ya Kwenda hospitali kufanyiwa vipimo ndipo tulipompeleka kituo cha afya Kaigara kwa ajili ya huduma za kitabibu, na baada ya hapo, tuliambiwa mtuhumiwa amekimbilia kusikojulikana,” amesema.

Ameongeza kuwa baada ya siku kadhaa, kaka na rafiki wa mtuhumiwa walifika nyumbani kwake wakiomba suala hilo limalizwe kifamilia ili mtuhumiwa arejee kazini, lakini alikataa ombi lao.

Naye mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Isaya Mbenja amesema amepokea taarifa hizo na halmashauri itaendelea na hatua ya kupelekwa taarifa za tuhuma hizo ili mamlaka zianze kufanya ufuatiliaji.

 

Chanzo: Nipashe

Send this to a friend