
Mwalimu Enock Johnson Peter (32) wa Shule ya Msingi Potwe wilaya ya Muheza mkoani Tanga amefariki dunia nyumbani kwake baada ya kukutwa amejinyonga na shuka, huku chanzo kikitajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema tukio hilo lilitokea Jumanne ya Julai 15, 2025 katika Kata ya Potwe na uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo ni wivu wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa Rajabu Msuya, Mratibu Elimu Kata ya Pongwe, waligundua kutokuwepo kwa mwalimu Enock katika kikao cha walimu kilichofanyika leo Jumatano, Julai 16, 2025. Mwanafunzi alitumwa kwenda kumuita lakini hakupata majibu. Baadaye mwalimu mwenzake alipochungulia dirishani, alikuta mwalimu huyo amejinyonga.
Abdulrazaq Kikungo, mmoja wa mashuhuda, amesema kuwa siku mbili kabla ya tukio, mwalimu huyo aligombana na mpenzi wake baada ya kukuta meseji za mapenzi kwenye simu ya mwanamke huyo, na kutishia kumchoma kisu.
Mwili wa mwalimu utaagwa shuleni hapo na kusafirishwa kupelekwa nyumbani kwao Ngara Kagera kwa ajili ya shughuli za mazishi.








