
Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora linamshikilia Torbeth Peter (39) mwalimu wa shule ya Sekondari Kata ya Igurubi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha Tatu wa shule hiyo.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Kanisia Mvula amesema tukio hilo limetokea Septemba 5, mwaka huu ambapo siku hiyo mzazi wa mwanafunzi huyo alifika shuleni ili kumuulizia akidai kuwa hakulala nyumbani, na baada ya mwanafunzi huyo kuhojiwa alisema alikuwa kwa mwalimu huyo.
Ameongeza kuwa alipopata taarifa za kukamatwa kwa mwalimu huyo alikwenda hadi kituoni na kumdhamini, lakini baadaye aliamua kufuta dhamana hiyo baada ya kubaini kuwa alifanya makosa kumdhamini mtuhumiwa huyo kwani kitendo hicho ni cha aibu na kisichokubalika kwenye jamii.
Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema bado wanaendelea na upelelezi kuhusu tukio hilo na kwamba mtuhumiwa huyo atafikishwa kizimbani mara baada ya upelelezi kukamilika.








