Mwalimu Mkuu ahukumiwa miaka 30 jela kwa kumbakaji, kumlawiti mwanafunzi

0
1

Mahakama mkoani Mara imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Masahunga, Wilayani Bunda, mkoani humo, Vicent Nkunguu, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumlawiti mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 16.

Hukumu hiyo imetolewa Aprili 23, 2025 na Hakimu Mwandamizi, Betron Sokanya, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, ambapo amesema kwa upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano, akiwemo mwanafunzi huyo na daktari aliyefanya uchunguzi wa kitabibu, pamoja na kielelezo kimoja.

Kwa upande wa utetezi, walileta mashahidi wawili akiwemo mke wa mshtakiwa na mwalimu mwenzake bila kuambatanisha vielelezo vyovyote.

Aidha, Mahakama pia imeamuru mshtakiwa kumlipa fidia ya shilingi milioni mbili mwathirika ambaye ni mwanafunzi anayesoma katika shule hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, pamoja na Kifungu cha 348(1) cha Sheria ya Uendeshaji wa Makosa ya Jinai.

Hakimu ameeleza kuwa wakati wa tukio, mwanafunzi huyo alifika nyumbani kwa mwalimu huyo kufuatia ombi la mke wa mwalimu huyo, kutokana na undugu wa kifamilia ambapo alitakiwa kuwapikia chakula watoto, kwani mama huyo alikuwa anakwenda kanisani. Baada ya shughuli kumalizika, walikula chakula cha usiku na kulala, ndipo tukio hilo lilipotokea.