Mwamvita Makamba aachana na kampuni ya Vodacom

0
51

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Mambo ya Nje wa Kampuni ya Vodacom, Mwamvita Makamba ameachana na kampuni hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka 14.

Kupitia taarifa yake aliyoitoa kwenye ukurasa wake wa LinkedIn, Mwavita amesema anajivunia miaka 14 aliyofanya kazi na Vodacom, moja ya kampuni kubwa za mawasiliano barani Afrika.

“Kutokana na uhusiano wa kifamilia tuliojenga na imani ambayo viongozi wangu walikuwa nayo kwangu, ulikuwa ni uamuzi mgumu kuondoka katika familia hii, moja ya maamuzi magumu zaidi ambayo nimelazimika kufanya. Lakini miaka 14 ni muda mzuri, na nimejitosheleza” imesomeka sehemu ya taarifa yake

Ameongeza kuwa “Kuwa sehemu ya maono ya Vodacom ya kutumia teknolojia kuunganisha vitu na watu kwa mustakabali bora, huku kutatua changamoto kubwa za kibinadamu katika masoko, imekuwa ni heshima kubwa.”

Katika miaka yake 14 na Vodacom, alianzisha mipango kadhaa ya kampuni hiyo barani Afrika ikiwa ni pamoja na M-Mama, mradi wa usafiri wa dharura unaolenga kusaidia akina mama na watoto wachanga kupata huduma muhimu ya kuokoa maisha katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania.

Kabla ya nafasi hiyo, Makamba alishikilia nafasi kadhaa katika kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara ya Pan Africa kwa Vodacom Business Africa na Kitengo cha Makampuni, Meneja Mtendaji Masuala ya Kampuni na Mdhamini wa Vodafone Foundation, Mkurugenzi wa Masuala ya Kampuni, Afisa Mkuu wa Masuala ya Kampuni, Biashara, na Mauzo ya Kampuni kati ya nyinginezo.

Send this to a friend