
Hali ya huzuni imetanda katika kijiji cha Rabuor, Kamsama, Kaunti ya Homa Bay nchini Kenya baada ya mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 13 kubakwa na kuuawa kikatili.
Mwili wa Mary Treza, mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Kamsama Comprehensive, umepatikana kando ya barabara siku ya Jumanne baada ya kupotea Jumatatu mchana.
Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Mbita, Peter Mutiso, amesema msichana huyo alivamiwa na watu wasiojulikana mara baada ya kuagana na wenzake akielekea nyumbani. Polisi wamesema mwili wake ulikutwa ukiwa umemwagiwa tindikali usoni na sehemu za siri.
Mbunge wa Suba North, Millie Odhiambo, amelaani kitendo hicho akikitaja kuwa cha kinyama na cha kushtua, na kuitaka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuchukua hatua za haraka ili kuwakamata na kuwachukulia hatua wote waliohusika.








