Mwanafunzi atembea zaidi ya kilomita 50 kwenda shuleni

0
41

Marisela Muthoni mwanafunzi anayetoka kwenye familia duni katika kijiji cha Gaseuni, Kaunti ndogo ya Tharaka-Nithi nchini Kenya, na kufanya vizuri katika mtihani wa elimu ya msingi (KCPE) kwa kupata alama 301, ametembea zaidi ya kilometa 50 kutoka nyumbani kwao mpaka shuleni alikochaguliwa kujiunga elimu ya sekondari.

Mwanafunzi huyo alieleza kwamba, ilimbindi aondoke nyumbani saa 11 alfajiri na kufika shuleni katika kitongoji cha Kaunti ya Tharaka-Nithi saa 8 mchana akiwa amevalia sare za shule ya Msingi ya Gaceuni, mkononi akiwa na barua ya kujiunga na kidato cha kwanza bila kuwa na sare za shule wala ada akidai mama yake ni mgonjwa na ndugu zake hawakuweza kumlipia karo.

Akizungumza na vyombo vya habari, Muthoni amesema hakuwa amekula chochote tangu asubuhi na usiku uliopita familia ililala njaa, hivyo alipokuwa akitembea kuelekea shule ilimbidi asimame mara kadhaa na kupumzika baada ya kuchoka sana, lakini mtu asiyemfahamu alimbeba kwenye pikipiki kwa takribani kilomita tano hadi soko la Gatunga.

“Niliamua kutembea hadi shuleni na kuomba uongozi uniruhusu kusoma huku nikiendelea kutafuta mtu wa kunisaidia” ameeleza Muthoni.

Amesema baada ya kufanya mtihani wa KCPE, alianza kutafuta pesa za karo lakini ilimbidi kuzitumia kununua chakula cha familia.

Msimamizi wa shule hiyo, Livingston Ali alisema msichana huyo atapata ufadhili kamili wa masomo kwa miaka hiyo minne.

“Msichana huyo ni mhitaji sana na tutamruhusu kusoma bila kulipa karo kwa miaka minne ijayo,” amesema Ali.

Send this to a friend