Mwanafunzi adaiwa kumwagia mwenzake tindikali kisa amekataa wasirudiane

0
35

Mwanafunzi kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Rift Valley (RVTTI) nchini Kenya, Tonny Kangor (24) amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka ya kumsababishia madhara ya kimwili aliyekuwa mpenzi wake kwa kumwagia tindikali (salfuric acid).

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Kangor alikasirishwa baada ya aliyekuwa mpenzi wake, Evaline Jelimo Sum (23), mwanafunzi mwenzake chuoni, kukataa kurejesha uhusiano wao baada ya kuachana kwa miezi kadhaa.

Inadaiwa kuwa asubuhi ya siku ya tukio, mshtakiwa alimvizia mwathirika alipokuwa akitembea peke yake kutoka nyumbani kwake alipokuwa amepanga kuelekea chuoni, ambako wote wawili walikuwa wamepangiwa kufanya mtihani wao wa mwisho.

Mahakama imeelezwa kuwa Kangor alimwita Evaline asimame ili wazungumze na kusuluhisha tofauti zao, lakini alikataa akieleza kuwa hana tena nia ya kuendeleza uhusiano wao. Hatua hiyo inadaiwa kumkasirisha mshtakiwa, ambaye alitoa kemikali aliyokuwa ameificha kwenye sweta yake na kumwagia kichwani na shingoni kabla ya kutoroka eneo la tukio.

Mwathirika alikimbizwa hospitalini akiwa na majeraha makubwa, huku polisi wakifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na baadaye kufikishwa mahakamani. Mshtakiwa amekana mashtaka hayo.

Send this to a friend