Mwanafunzi wa chuo ajifungua na kumtupa mtoto nyuma ya nyumba

0
37

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza aliyetambulika kwa jina moja la Judith amenusurika kipigo kutoka kwa wananchi akidaiwa kujifungua na kumtupa mtoto nyuma ya nyumba anayoishi.

Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo anayesoma shahada ya sheria mwaka wa tatu chuoni hapo, alitekeleza tukio hilo asubuhi ya Juni 20, mwaka huu nyumbani kwake mtaa wa Silivin Sweya jijini Mwanza.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Silivini, Rajabu Ramadhan amethibitisha kutokea tukio hilo akibainisha kuwa mtuhumiwa huyo yupo chini ya ulinzi wa polisi kwa mahojiano zaidi.

“Baada ya kukuta mwili wa kichanga umetupwa tulifanya msako wa kujua mtu aliyekuwa na ujauzito na tulimbaini mwanafunzi wa SAUT ambaye baada ya kumchunguza tumekuta ana dalili za kutoa mimba kwani alikuwa akitokwa na damu,” amesema.

Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Felister Severine amesema amebaini kuwepo tukio hilo baada kusikia kelele za mtuhumiwa akilalamika kupata maumivu ya tumbo jambo lililomfanya atoke nje na kukutana na matone ya damu yaliyoanzia katika mlango wa chumba cha mtuhumiwa hadi nje ya geti.

“Tulipotoka nje baada ya kusikia kelele tulikutana na matone kuanzia kwenye chumba chake hadi nje ya geti kufuatilia damu hiyo ndipo tukakutana na kichanga kilichokufa kikiwa kimetelekezwa nje ya geti,” amesema.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend