Mwanafunzi wa mwaka wa mwisho ajiua baada ya kusimamishwa chuo

0
146

Simanzi na huzuni zimetanda katika Chuo Kikuu cha Babcock nchini Nigeria kufuatia kifo cha Joshua Lawson (20), mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika kozi ya Sayansi ya Kompyuta, aliyeripotiwa kujitoa uhai baada ya kupewa adhabu ya kusimamishwa masomo kwa mwaka mmoja, kwa tuhuma za kufanya udanganyifu kwenye mtihani.

Lawson, ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne na alitarajiwa kuhitimu Julai 27, aliripotiwa kujiua nyumbani kwao Lagos, muda mfupi baada ya kuarifiwa kuhusu hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi yake na uongozi wa chuo hicho.

Akithibitisha tukio hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko wa Chuo Kikuu cha Babcock, Dkt. Joshua Suleiman, amesema Lawson alipatikana na hatia ya kufanya udanganyifu katika mtihani na kamati ya nidhamu ya chuo hicho baada ya kuhojiwa.

“Alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Sayansi ya Kompyuta. Alifikishwa mbele ya kamati ya nidhamu na akapatikana na hatia ya kufanya udanganyifu. Alipewa adhabu ya kusimamishwa kwa mwaka mmoja. Ingawa hakuwa amepokea barua rasmi ya kusimamishwa, inaonekana alishapata taarifa kuhusu uamuzi huo,” amesema.

Taarifa hiyo imezua hasira mitandaoni, ambapo watu mbalimbali wamehoji ukali wa sera za kinidhamu za chuo hicho.

Send this to a friend