
Mwanaharakati wa Haki za Binadamu nchini Kenya, Boniface Mwangi amekamatwa kwa tuhuma zinazohusishwa na ugaidi na kuchoma mali ya umma kwa makusudi.
Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Binadamu la Vocal Africa, Hussein Khalid amethibitisha kukamatwa kwake huku mamlaka zikidai kuwa mwanaharakati huyo anachunguzwa kuhusiana na ghasia zilizoambatana na maandamano ya Juni 25 na Julai 7.
Aidha, video zilizosambazwa na mke wa Mwangi, Njeri Mwangi, kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), zinadai kuwa maafisa wanaodaiwa kuwa polisi walivamia makazi ya wanaharakati hao, maarufu kama Courage Base, wakafanya upekuzi na kuchukua vifaa vya kielektroniki ikiwemo simu.
“Wamechukuwa simu na tarakilishi zake zote wakisema kwamba wanampeleka katika makao makuu ya idara ya uchunguzi wa jinai, DCI. Ninashindwa kupumua” ameandika Njeri.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, alisema wiki hii kuwa zaidi ya watu 1,500 wamekamatwa kwa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na uhaini, ugaidi, ubakaji na uharibifu wa mali ya umma.







