Mwanamke ahukumiwa maisha kwa kuwaua wazazi wake na kuishi na miili yao kwa miaka minne

0
61

Mwanamke mmoja anayejulikana kwa jina la Virginia McCullough amefungwa jela maisha baada ya kuwaua wazazi wake wote wawili na kuishi na miili yao kwa miaka minne ndani ya nyumba ya familia.

Virginia mwenye umri wa miaka 36, alimuua baba yake, John mwenye umri wa miaka 70, kwa kumtilia sumu kupitia dawa za hospitali, kisha kumchoma kisu kifuani mama yake Lois, mwenye umri wa miaka 71 katika nyumba yao iliyopo Chelmsford, Essex nchini Uingereza.

Taarifa zinaonyesha kwamba vifo vya wazazi wake vilitokea mnamo Juni 2019, lakini miili yao haikugundulika hadi 2023 baada ya daktari wao kutoa taarifa ya kutoonekana kwao katika miadi ya kawaida.

Mwanamke huyo alikuwa akiwaambia marafiki na majirani kwamba wazazi wake walikuwa wamehamia mbali, walikuwa wagonjwa, au walisafiri kwa muda mrefu.

Baada ya maafisa kufika katika nyumba hiyo, mwanamke huyo aliwaambia maafisa kwamba yuko tayari kushirikiana nao kwani alijua siku ya kukamatwa kwake ingewadia, ambapo aliwaelekeza sehemu ambapo miili hiyo ipo na kuwaonesha kisu kilichotumika kumuua mama yake.

Mwendesha mashitaka, Lisa Wilding KC aliambia mahakama kwamba McCullough alitengeneza kaburi la muda kwa ajili ya baba yake, ambalo lilifunikwa na blanketi nyingi na picha kadhaa juu yake katika chumba ambacho kilikuwa ni ofisi ya baba yake huku mwili wa mama yake, ukiwekwa kwenye mfuko ndani ya kabati katika chumba cha kulala cha mama yake kilichokuwa juu ya nyumba.

Send this to a friend