Mwanamke aishi na wembe tumboni kwa miaka 11

0
38

Madaktari nchini Kenya wameondoa wembe unaodaiwa kusahaulika ndani ya tumbo la mwanamke kwa muda wa miaka 11 baada ya upasuaji uliofanyika katika hospitali ya Kitale, Magharibi mwa Kenya wakati wa kujifungua.

Felistah Nafula (36), amekuwa akiishi na maumivu ya tumbo ambayo aliamini ni vidonda vya tumbo ambavyo amekuwa akipatiwa matibabu, na ndipo madaktari waliposhuku kuwa inawezekana tatizo lake ni kubwa kuliko ilivyodhaniwa.

Uchunguzi uliofanyika mara kadhaa ulionesha Bi. Felistah alikuwa akisumbuliwa na kitu tumboni mwake na kisha kulazwa katika hospitali ya Maragua Level Four katika Kaunti ya Murang’a.

Dkt. Kairo Kimende, msimamizi wa matibabu wa hospitali hiyo aliongoza timu ya upasuaji uliofanyika kwa masaa mawili na kuuondoa wembe uliopatikana kwenye tumbo uliokuwa kati ya uterasi na utumbo mwembamba.

Aidha, Dkt. Kimende amesema wembe huo ulikuwa umetanda kwa njia ambayo ulisababisha mwanamke huyo apoteze uwezo wa kubeba mimba kwa muda mrefu, huku Bi Nafula akidai kuwa tatizo hilo lilikaribia kuvunja ndoa yake kwa kuwa mumewe hakuelewa ni kwanini hawakupata mtoto kwa muda wa miaka 10.

Send this to a friend