Polisi wilayani Mubende nchini Uganda wanachunguza madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa baada ya kudaiwa kutoa figo ya mama aliyejifungua wakati akiwa hajitambui.
Imeelezwa kuwa Peragiya Muragijemana (20), mkazi wa Kijiji cha Lwemiggo, Wilaya ya Mubende amesema baada ya kujifungua mikononi mwa mkunga wa jadi alishindwa kutoa kondo la nyuma na kutokwa damu nyingi ndipo alikimbizwa hospitalini akiwa katika hali mbaya.
Awali baada ya kufikishwa hospitalini hapo madaktari walimueleza mume wa Peragiya, Amos Tiringanya kuwa mkewe anahitaji kufanyiwa upasuaji, hivyo alitakiwa kusaini hati ya kumruhusu kufanyiwa upasuaji huo.
Tiringanya ameeleza kuwa Peragiya aliruhusiwa baada ya siku tatu kutokana na msongamano hospitalini hapo, lakini baada ya siku tatu alitaarifiwa na mama yake Peragiya kuwa amepata matatizo ya tumbo.
“Tulienda kwenye uchunguzi wa hali ya juu zaidi ambao ulionesha kuwa figo yake ya kulia haikuwepo. Nilitia saini tu hati inayokubali kuondolewa kwa uterasi ya mke wangu ili kuokoa maisha yake, si figo yake,” alisema Tiringanya
Hata hivyo Msimamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mubende, Onesmus Kibaya ameishauri familia hiyo kuwa watulivu kwani hospitali hiyo inafanya uchunguzi wake, na kuongeza kuwa hospitali hiyo haina uwezo wa kufanya upasuaji wa figo.