Mwanamke aliyemuuza bintiye kwa mganga ahukumiwa kifungo cha maisha jela

Mwanamke aliyemteka na kumuuza binti yake wa miaka sita akiwa na washirika wake wawili nchini Afrika Kusini, amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Racquel “Kelly” Smith (35), pamoja na mpenzi wake, Jacquen Appollis na rafiki yao, Steveno van Rhyn, walishirikiana kumuuza mtoto huyo kwa mganga wa kienyeji ambaye alivutiwa na macho ya mtoto huyo pamoja na rangi ya ngozi yake.
Mama huyo alikiri kumuuza binti yake kwa mganga wa kienyeji Februari 2024 kwa Randi 20,000 [TZS takriban milioni 3].
Licha ya msako mkubwa na umaarufu wa tukio hilo, mtoto huyo, Joshlin Smith ambaye alipotea Februari 2024 huko Saldanha Bay, karibu na Cape Town, bado hakupatikana.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya kesi ya wiki sita iliyoibua hisia kubwa nchini humo, ambapo mashahidi na upande wa mashtaka walitoa ushahidi wao mahakamani hapo.
