Levina apanga njama ya kutekwa na kuporwa milioni 8 ya mwajiri

0
4

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya limekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kumshikilia mwanamke mmoja aitwaye Levina Matala (25), mkazi wa Kabwana, ambaye aliripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana Februari 17, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, inadaiwa kuwa siku ya tukio, majira ya mchana katika Kijiji cha Kabwana, Wilaya ya Kipolisi Shirati, Levina alitekwa akiwa nje ya benki na kuporwa shilingi milioni nane, mali ya mwajiri wake, Nguka Kitori, ambaye ni mmiliki wa biashara ya miamala ya fedha. Baada ya tukio hilo, Levina alitelekezwa katika Kijiji cha Utegi.

Hata hivyo, uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi ulibaini kuwa tukio hilo lilipangwa, ambapo Levina alikuwa sehemu ya mpango huo pamoja na mshirika wake, Edwin Malaki (45), mkazi wa Shirati.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya liliwakamata watuhumiwa hao na baadaye kumuachia kwa dhamana mtuhumiwa Levina mnamo Februari 19, 2025, huku uchunguzi wa shauri hilo ukiendelea,” ilisema taarifa ya Polisi.

Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kupuuza taarifa za uzushi na upotoshaji zinazoweza kuleta taharuki.

Send this to a friend