Mwanamke apatikana na hatia ya kuua familia ya mume wake wa zamani

0
146

Erin Patterson (50) kutoka Leongatha, jimbo la Victoria kusini mwa Australia, amepatikana na hatia ya mauaji ya wazazi wa mume wake wa zamani na shangazi wa mume wake baada ya kuwalisha chakula kilichochanganywa na uyoga wenye sumu kali.

Tukio hilo lilitokea Julai 29, 2023, baada ya Erin kuwaalika nyumbani kwake wazazi hao, Don na Gail Patterson (wote miaka 70) pamoja na Heather Wilkinson (66) na mumewe, Mchungaji Ian Wilkinson kwa chakula cha mchana.

Baada ya kula, wote wanne waliumwa sana. Don na Gail pamoja na Heather walifariki siku chache baadaye, na mume wa Heather alinusurika lakini alikaa hospitalini kwa wiki saba.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Erin alitumia uyoga wa sumu wa Amanita phalloides, ambao una sumu inayoweza kuua kwa muda mfupi. Ushahidi umeonesha kuwa wageni walipewa chakula kwenye sahani kubwa za kijivu, huku Erin mwenyewe akila kwenye sahani ndogo ya rangi ya kahawia.

Mchungaji Wilkinson amefichua kuwa baada ya chakula, Erin alidai kuwa ana saratani na alitaka msaada wa jinsi ya kuwaambia watoto wake kuhusu hali hiyo, madai yaliyobainika kuwa ya kutungwa.

Aidha, inaripotiwa kuwa mume wake wa zamani na baba wa watoto wake wawili, Simon Patterson alikuwa amealikwa kwenye mlo huo lakini alikataa kuhudhuria.

Erin Patterson amekuwa rumande tangu alipokamatwa Novemba 2023, na sasa amepatikana na hatia rasmi. Hukumu yake kamili inasubiriwa kutolewa na mahakama.

Send this to a friend