Mwanamke mmoja kutoka nchini Uganda mwenye umri wa miaka 70 amejifungua mapacha baada ya kupata ujauzito kupitia matibabu ya kupandikiza (IVF), na kuweka rekodi ya mwanamke mzee zaidi barani Afrika kujifungua.
Kituo cha Kimataifa cha Hospitali ya Wanawake na Kituo cha Uzazi katika mji mkuu wa Uganda kimesema mwanamke huyo anayejulikana kama Safina Namukwaya amejifungua mapacha wa kike na wa kiume.
Kwa mujibu wa Namukwaya, mapacha hao ni uzao wake wa pili baada ya kujifungua mtoto wa kike mwaka 2020 huku akieleza changamoto alizopitia katika kipindi cha ujauzito ikiwemo kutengwa na baba wa watoto hao.
“Wanaume hawapendi kuambiwa umebeba zaidi ya mtoto mmoja, tangu nilipolazwa hapa hajawahi kufika,” amesema.
Aidha, amesema anafurahi kupata watoto baada ya miaka mingi ya kuvumilia unyanyapaa na kejeli za kukosa watoto japokuwa hajui namna atakavyoweza kuwalea watoto hao.