Mwanamuziki ajitoa tuzo za AFRIMMA baada ya kushambuliwa kwa kupigia kampeni chama tawala

0
19

Mwanamuziki kutoka Zambia, Slapdee amejitoa kwenye kuwania tuzo za muziki baada ya kushambuliwa na mashabiki kutokana na kutumbuiza kwa kilichokuwa chama tawala nchini humo, The Patriotic Front, ambacho kiling’olewa madarakani Agosti 2021.

Nyota huyo ambaye jina lake ni Mwila Musonda awali alitetea uamuzi wake wa kutumbuiza kuwa ilikuwa ni biashara, lakini utetezi huo haukufanya mashabiki hao wamwache.

Baada ya kutajwa kwenye tuzo za AFRIMMA, jamii ya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Zambia ilisema watampigia kura mshindani wake kutoka Afrika Kusini, Cassper Nyovest katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume Kusini mwa Afrika. Sehemu ya waliopo kwenye kipengele hicho ni pamoja na Jah Prayzah kutoka Zimbabwe na The Dogg kutoka Namibia.

Kampeni hiyo ambayo ilikuwa ikimuinua Cassper Nyovest ilikuwa miongoni mwa mambo gumzo (trending) nchini Zambia jana.

“Nimeelewa, nilichukulia ushawishi wangu kwa urahisi na kufanya uamuzi wa kibinafsi. Niliwaangusha watu ambao nilitakiwa kuwapigania na kuwa upande wao. Kwa hilo, kweli naomba radhi. Siandiki hili ili kupata huruma yenu kuhusu mchakato wa tuzo unaoendelea, lakini kuwa na amani na maisha matulivu na wale wote niliowaumiza. Ni kweli makosa yalifanyika, na nimejifunza somo,” ameandika Slapdee kwenye ukurasa wake wa Facebook (tafsiri ya mwandishi).

Amesema ameiomba menejimenti yake kumwondoa haraka kwenye orodha ya wanaowania tuzo za AFRIMMA kwa sababu hakuna mantiki ya kushinda tuzo kama huwezi kushinda nyoyo za watu wako.

Hii si mara ya kwanza kwa wanamuziki nchini humo kutumbuiza kwenye shughuli za kisiasa hasa zinazohusu chama tawala.

Tuzo za AFRIMMA zinatarajiwa kutolewa Novemba 21 mwaka huu.

Send this to a friend