Mwanamume mmoja aliyetambulika kwa jina la Michael Okurut (39) anazuiliwa na polisi baada ya kukamatwa kwa madai ya kumpiga Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Musa Ecweru wakati wa misa ya Jumapili katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Michael Kaunti Ndogo ya Wera, Wilaya ya Amuria nchini Uganda.
Inadaiwa kuwa mwanaume huyo alimpiga waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Kaunti ya Amuria, katikati ya hotuba yake kwa waumini wa kanisa hilo.
“Alikuja kimya kimya na hata kufanya ishara ya msalaba. Nilifikiri angetafuta kiti ili akae kama walivyokuwa wakifanya waumini wengine lakini badala yake alienda kwa waziri na kunong’ona kabla hajampiga waziri kofi zito sikioni,” kilisema chanzo kimoja.
Baada ya tukio hilo idaiwa kuwa mwanaume huyo alijaribu kumpiga kofi la pili na ndipo walinzi wa Waziri Ecweru walipomkamata kwa nguvu na kumkabidhi kwa polisi wa eneo hilo.
Oscar Ageca, Kaimu Msemaji wa Polisi wa Kyoga Mashariki amesema, Okurut alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Wera kwa mahojiano.
Chanzo cha habari kinasema Waziri Ecweru alipowasiliana na chombo hicho cha habari nchini humo alidai kuwa mshukiwa ni mgonjwa wa akili.