Mwanasheria Mkuu: Kuna upotoshaji mkubwa suala la bandari

0
43

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi, amesema kuna upotoshaji mkubwa usio na tija katika mijadala inayoendelea kuhusu suala la uwekezaji wa kampuni ya Dubai ya DP World unaotarajiwa kufanyika kwenye bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dodoma, Jaji Feleshi amesema kuwa upotoshaji huo unaweza kuifanya Tanzania ionekane kama inabagua wawekezaji kutoka nchi fulani na kuharibu sifa ya Tanzania kama taifa linaloongoza kuvutia watalii kwenye ukanda huu wa Afrika.

“Mtu anasema mkataba ni wa miaka 100 na hiyo ilikuja hata kabla Bunge halijaazimia. Wengine wanasema ni mkataba wa maisha. Unatafuta hicho kipengele cha maisha unapekua kifungu kimoja mpaka mwisho, hakuna,” amesema Feleshi.

Aidha, Mwanasheria Mkuu pia amekanusha kuwa bandari ya Dar es Salaam inauzwa kwa kusema kuwa hakuna kipengele chochote kwenye mkataba kati ya Tanzania na Dubai (intergovernmental agreement au IGA) kinachozungumzia uuzwaji wa Bandari.

Pia amefafanua kuwa Bunge limepitisha azimio la Ushirikiano kati ya Serikali ya Dubai na Tanzania kwenye eneo la bandari, lakini hakuna mkataba wowote ambao umesainiwa kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya DP World.

Mbali na hayo, amekanusha taarifa zinazoenezwa na baadhi ya watu kwamba Tanzania au TPA haitaweza kujitoa katika makubaliano itakayoingia na DP World, na kwamba mwekezaji huyo atapewa masharti mahsusi na malengo ya utendaji, na endapo mwekezaji ataonesha ufanisi, ataweza kuongezewa maeneo mengine kwa mujibu wa matakwa ya serikali.

Send this to a friend