Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakiwa kuhakikisha serikali inashinda kesi
Rais Dkt. Magufuli amemuapisha Prof. Adelardus Lubango Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akizungumza baada ya kumuapisha, Rais Magufuli amesema Watanzania wana matumaini makubwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanataka kuona Serikali yao inapata uwakilishi mzuri katika masuala ya kisheria, hivyo amemtaka kuhakikisha anasimamia vizuri kesi za Serikali na kuzitetea kwa uharaka mali za Serikali.
“Watanzania hawapendi kuona Serikali yao inashindwa katika kesi, kachape kazi, kawatetee Watanzania hasa wanyonge, katetee mali za Serikali na kwa haraka. Umefanya kazi nzuri katika kipindi chako cha kwanza, nataka ukafanye kazi vizuri zaidi, ukajipange sawasawa, ndio maana nakupongeza lakini wakati huo huo nakupa pole kwa majukumu haya,” amesema Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amewatoa hofu viongozi wateule wote ambao wamekuwa na hofu ya kuondolewa ama kubadilishwa katika nafasi walizonazo baada ya yeye kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili, akisema hatarajii kufanya mabadiliko ya viongozi hao labda kwa wale watakaokuwa wanastaafu ama kutofanya vizuri katika majukumu yao.
“Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi, Viongozi wa Taasisi na Idara za Serikali na wengine wote chapeni kazi, simuondoi mtu kwenye nafasi yake labda aharibu yeye mwenyewe au astaafu” amesisitiza Rais Magufuli.