Mwanaume aliyetuma wanaume 50 kumbaka mke wake akiri mashitaka

0
78

Mwanaume mmoja nchini Ufaransa anayeshtakiwa kwa kumuwekea dawa za kulevya mke wake na kuwaruhusu wanaume takribani 50 kumdhulumu kingono akiwa amelala katika vipindi tofauti huku akirekodi matukio hayo, amekiri mashitaka yote mahakamani.

Dominique Pelicot, mwenye umri wa miaka 71 anadaiwa kuwaalika wanaume hao nyumbani kwake na kuwaelekeza jinsi ya kumfanyia ubakaji mke wake bila yeye kuamka, akiwataka wasivute sigara au kutumia manukato ili asijue kilichokuwa kikiendelea.

Mke wake, Gisele Pelicot aliyezaa naye watoto watatu, amekubali kutoficha utambulisho wake huku akieleza mahakamani kuwa kwa miaka 50 aliishi na mwanaume huyo bila kufikiria angeweza kufanya ukatili huo.

Akiwa kizimbani huko Avignon, Kusini-mashariki mwa Ufaransa, Dominique ameonesha kujutia matendo yake, akiomba msamaha, ingawa amekiri kuwa anajua kuwa matendo hayo hayawezi kusamehewa.

“Mimi ni mbakaji kama wengine wote katika chumba hiki. Walijua kila kitu. Naomba mke wangu, watoto wangu, wajukuu zangu wapokee msamaha wangu. Najuta nilichofanya. Nakuomba msamaha, hata kama hausameheki,” amesema.

Dominique alikamatwa mwaka 2020 baada ya tukio lingine ambapo mlinzi wa duka alimtuhumu kwa kumrekodi kwa siri mwanamke ndani ya duka. Polisi walipopekua nyumba yake na vifaa vyake vya kielektroniki, walikuta maelfu ya picha na video za wanaume wakifanya vitendo vya kingono na mke wake wakati akionekana hajitambui ndani ya nyumba yao.

Send this to a friend