Mwandishi wa habari wa Marekani akamatwa Urusi kwa madai ya ujasusi

0
39

Mwandishi wa habari wa Marekani, Evan Gershkovich amekamatwa nchini Urusi kwa shutuma za ujasusi alipokuwa akifanya kazi na jarida la Wall Street Journal.

Gershkovich (31) anajulikana sana miongoni mwa waandishi wa habari wa kigeni mjini Moscow akitajwa kuwa ripota bora na mwanahabari mashuhuri mwenye kufuata kanuni za kazi.

Jarida la Wall Street Journal limesema mwandishi wake aliacha kuwasiliana na wahariri wake alipokuwa akifanya kazi huko Yekaterinburg, karibu kilomita 1,600 (maili 1,000) mashariki mwa Moscow, Jumatano alasiri.

Maafisa wa Marekani wamesema dereva wa Gershkovich alimuacha kwenye mgahawa na baadaye simu yake ilikuwa imezimwa, hivyo jarida hilo liliajiri wakili kujaribu kumtafuta katika makao makuu ya FSB jijini, lakini walimweleza wakili huyo kuwa hawana taarifa zake.

Kulingana na idara ya usalama ya FSB ya Urusi, mwandishi huyo wa habari alikuwa amezuiliwa kutokana na kukusanya taarifa zilizoainishwa kama siri ya serikali kuhusu shughuli za shirika la ulinzi la Urusi wakidai kuwa alikuwa akitekeleza maagizo ya Marekani.

Ujasusi nchini Urusi adhabu yake ni kifungo cha juu cha miaka 20 jela. Shirika la habari la Tass limeripoti kwamba mwanahabari huyo amekana shitaka hilo.

Send this to a friend