Mwandishi wa habari wa Reuters jela kwa kueneza habari za uongo

0
41

Mahakama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imemhukumu kwenda jela miezi sita mwandishi wa habari wa nchini humo, Stanis Bujakera baada ya kumtia hatiani kwa kueneza habari za uongo.

Mbali na adhabu hiyo, mwanahabari huyo ambaye anafanya kazi katika vyombo vya habari vya kimataifa ikiwa ni pamoja na jarida la Jeune Afrique na Reuters ameamuriwa kulipa faini ya TZS 928,000.

Bujakera, ambaye alikana mashtaka yote, alikamatwa katika mji mkuu Kinshasa kwa tuhuma za kueneza habari za uongo kuhusu mauaji ya mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, katika makala iliyochapishwa na Jeune Afrique, gazeti la habari la Ufaransa limesema.

Akizungumza na vyombo vya habari wakili wa Bunjera, Jean-Marie Kabengela amesema mwanahabari huyo anatarajia kuondoka katika gereza ambalo amekuwa akishikiliwa tangu Septemba mwaka jana kwa sababu tayari ameshatumikia muda huo.

Mwendesha mashtaka katika kesi hiyo mapema mwezi huu aliitaka mahakama ya Kinshasa kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela huku mashirika ya haki za ndani na kimataifa yakilaani kushikiliwa kwake, wakiliita tukio hilo kuwa ni shambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya Habari.

Send this to a friend