Mwanza: Magari yasimamishwa kwa saa nne ili Makamu wa Rais apite

0
41

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amesema amesikitishwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kufunga barabara kwa saa nne katika msafara wake jijini Mwanza na kuagiza kitendo hicho kisijirudie tena.

Akizungumza wakati akisalimiana na wananchi katika ziara yake jijini humo, Dkt. Mpango amewaomba radhi wananchi kwa tukio hilo na kuwaagiza wote watakaohusika kuupokea msafara wake katika maeneo mbalimbali kufanya mawasiliano ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao.

“Mambo ya kufunga barabara kwa masaa [saa] mengi kwa sababu tu mtoto wa masikini anaitwa Philip Mpango anapita hapa, hapana. Jana naambiwa mmefunga barabara mpaka masaa manne haiwezekani, kwanini? Sitaki kusikia tena hili linajirudia, muambizane na hao watakaopokea msafara huko nitakakopita. Acheni wananchi wapite, kwani dakika 10 hazitoshi?” amesema.

Mbunge: Misafara ya viongozi inakwamisha shughuli za wananchi

Wakati wa kikao cha bunge cha Aprili 12, 2023 Mbunge Kunti Majala aliibua hoja juu ya misafara ya viongozi wa juu wa Serikali kutumia muda mrefu na kuwakwamisha wananchi katika shughuli zao, hivyo kuishauri Serikali kutafuta namna bora ya kudhibiti misafara hiyo.

Hata hivyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama alijibu hoja hyo akieleza kuwa misafara hiyo ipo kwa utaratibu maalum ambao pia unasimamia heshima kwa viongozi wa nchi.

 

Send this to a friend