Mwekezaji wa Misri aahidi kuleta wawekezaji 50 nchini

0
39

Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Elsewedy Electric kutoka nchini Misri, Mhandisi Ahmed El Sewedy ameahidi kuwa katika kipindi cha miaka 2 atahamasisha makampuni takribani 50 kutoka Misri kuja kuwekeza Tanzania.

Sewedy ametoa ahadi hiyo kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 13, 2021 alipofika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma kuzungumza na Rais.

Aidha, amesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuwekwa na Serikali, wameamua kuunga mkono na kuwekeza zaidi kwa kujenga eneo la viwanda lenye ukubwa wa mita za mraba milioni mbili ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha mbolea.

Katika mazungumzo hayo, Mhandisi  El Sewedy amemfahamisha Rais Samia kuwa kampuni yake mbali na kuwa miongoni mwa kampuni zinazojenga mradi wa kuzalisha umeme katika Bwala la Mwalimu Nyerere, pia imewekeza katika miradi mingine.

Pia amesema katika eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam, kampuni yake imejenga kiwanda cha kuzalisha nyaya za umeme, transfoma, vifaa vya kuzuia nyaya za umeme zisilete hitilafu na mita za umeme, ambacho kinatarajiwa kufunguliwa rasmi mwezi Disemba mwaka 2021. 

Kwa upande wake, Rais Samia amemshukuru Mhandisi El Sewedy  na kumuhakikishia kuwa Serikali itampa ushirikiano katika kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo kwa muda muafaka. 

Aidha, Mhe. Rais Samia amemjulisha Mhandisi huyo kuwa kwa sasa Tanzania inapitia sheria na sera zake mbalimbali ili kujenga mazingira mazuri zaidi ya biashara na uwekezaji.

Send this to a friend