Mwendesha Mashtaka aondoa rufaa dhidi ya Sabaya na wenzake

0
23

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imewasilisha ombi la kuiondoa rufaa Na. 155 ya mwaka 2022 dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake, ikisema haina tena nia ya kuendelea nayo.

Rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa mfululizo na Mahakama Kuu kuanzia Aprili 29 hadi Mei 03 mwaka huu mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi, mara baada ya Sabaya na wenzake kushinda kesi ya uhujumu uchumi Na. 27 ya mwaka 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha iliyosikilizwa na kuamuliwa na Hakimu Patricia Kisinda.

“Mheshimiwa Jaji, shauri hili limekuja kwa ajili ya kusikiliza rufaa. Hata hivyo, mrufani (Jamhuri) amewasilisha ombi chini ya kifungu cha sheria Na. 386 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, marejeo ya mwaka 2022, ombi letu ni kwamba Jamhuri haina nia ya kuendelea na rufaa hii dhidi ya Sabaya na wenzake, hivyo tunaomba kuiondoa hapa mahakamani,” ameeleza Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Akisa Mhando akiwasilisha nia ya kuondoa shauri hilo.

Akizungumza na waandishi wa Habari Wakili wa Sabaya, Moses Mahuna amesema kuanzia sasa, Sabaya ni mtu huru na kwa mujibu wa mahakama yenyewe, hana rekodi yotote ya uhalifu na hana shauri lingine lolote katika chombo chochote cha sheria.

Send this to a friend