Mwenezi BAWACHA Njombe adaiwa kushambuliwa na mlinzi wa CHADEMA

0
10

Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Sigrada Mligo, mkazi wa Mji mwema mkoani Njombe ameripotiwa kujeruhiwa na mlinzi wa chama hicho wakati wa kikao cha ndani kilichofanyika Machi 25, 2025, mjini Njombe, kikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, John Heche.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amethibitisha taarifa hizo ambapo kwa mujibu wa taarifa za polisi, kikao hicho cha ndani kilijadili masuala mbalimbali, ikiwemo hoja kuhusu Sigrada Mligo, kudaiwa kufanya mikutano bila kufuata utaratibu wa chama.

Kamanda Banga amesema katika hoja hiyo, kuliibuka taharuki na sintofahamu na baadaye Mligo alielekezwa kutolewa nje ya kikao ili kupunguza mvutano.

Ameeleza kuwa baada ya hali kutulia, aliruhusiwa kurejea katika kikao hicho. Hata hivyo, ghafla mmoja wa walinzi wa CHADEMA aliyejulikana kama Noel Olevale aliripotiwa kumshambulia, na kusababisha Mligo kuanguka chini. Askari waliokuwepo eneo hilo walijaribu kumkamata mtuhumiwa, lakini alifanikiwa kutoroka.

Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe lilifanya jitihada za kumpatia huduma ya kwanza ikiwemo kumpatia PF3 na kufungua kesi, na kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Kibena mkoani Njombe akiwa anaendelea kupatiwa matibabu huku jitihada za kumtafuta mtuhumiwa zikiendelea.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani halitosita kuchukua hatua kwa mtu yoyote atakayebainika kufanya hivyo.