Mwenyekiti UVCCM auawa baada ya kufumaniwa

0
42

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Ramadhani Hamisi (30) wa Kata ya Kaselya, Iramba mkoani Singida ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali tumboni baada ya kudaiwa kukutwa na mke wa Ally Athumani usiku wa Desemba 30, 2022.

Kwa mujibu wa gazeti la Raia Mwema, tukio hilo lililotokea katika Kitongoji cha Msisi linaelezwa kuwa marehemu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa Athumani, na walishakutwa mara kadhaa wakiwa pamoja na kupewa onyo juu ya tabia hiyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kaselya, Wazzael Majja amedai tukio hilo lilitokea majira ya saa nne usiku baada ya mtuhumiwa kuwakuta nyumbani kwake, na ndipo ulipoibuka ugomvi na kuanza kufukuzana gizani kisha kupotezana njiani, lakini mtuhumiwa alimvizia Ramadhani nyumbani bila yeye kujua na kumshambulia.

Baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa alikwenda kwa mzazi wa Ramadhani, Ally Hamis kumwambia akamwone mwanawe anakufa. “Mimi tayari kazi nimemaliza, nimemkuta mwanao anamchezea mke wangu,” anadaiwa kumweleza baba wa marehemu na kuondoka.

“Baba huyo alipotoka nje alimkuta mwanaye hajiwezi huku damu zikimvuja tumboni. Akiwa bado anafahamu alimwambia baba yake kuwa ‘nikifa nimeuawa na Ally, amenichoma kisu akakimbia’” amesema.

Ramadhani amefariki baada ya kufikishwa katika hospitali ya mkoa wa Singida, huku Polisi baada ya kufika katika eneo hilo siku ya Jumamosi, hawakuwakuta Athumani na mkewe kwani nao walikimbia usiku wa tukio.

Chanzo: Raia Mwema

Send this to a friend