Mwigulu awataka wafanyabiashara waliokimbilia Zambia kurejea, aahidi mwafaka

0
13

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wafanyabiashara wa Tanzania waliokimbilia Nakonde nchini Zambia kurejea na kufanyabiashara nchini na kuwahakikishia kuwa malalamiko yao kuhusu kodi yatafanyiwa kazi.

Dkt. Nchemba ametoa wito huo mjini Tunduma wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji huo wakiwemo wafanyabiashara katika mpaka wa Tanzania na Zambia

Wito huo umetokana na wafanyabiashara kueleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wenzao wamehamishia biashara zao upande wa Nakonde nchini Zambia wakidai kuwa kufanya biashara upande huo kuna nafuu ya kodi ikilinganishwa na upande wa Tanzania.

“Wewe ni Mtanzania usiikimbie nchi yako, tutarekebisha matatizo, lakini kama umepata fursa ya kuwekeza huko, wekeza! Laniki usiikimbie nchi yako kwa sababu ya matatizo. Tanzania inaheshima ya kuzikomboa nchi zote hizi, hatuwezi kushindwa kutenda haki kwa wananchi wetu,” ameongeza Dkt. Nchemba.

Aidha, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweka utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara mara kwa mara ili kutatua changamoto zinazowakabili pamoja na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kutoa stakabadhi za kielektroniki zikiwa na bei halali.

Amewaonya wafanyabiashara kuacha tabia ya kuuza huduma na bidhaa zao kwa kutumia bei za aina mbili; moja ikiwa ni kuwauzia wateja bidhaa bila kutoa risiti au kuandika kiasi kisichosahihi akibainisha kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na kwamba wakikamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Send this to a friend