Mwigulu: Tanzania bado ipo uchumi wa kati

0
47

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amekanusha takwimu zilizotolewa na Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo zilizoonesha kuwa Tanzania imeshuka kutoka uchumi wa kati kurudi katika uchumi wa chini.

Akijibu hoja hiyo bungeni jijini Dodoma, Dkt. Mwigulu amesema Benki ya Dunia huwa inatoa takwimu za ‘GNI per capital’ kwa nchi kila Julai Mosi wa mwaka ambapo takwimu zinazokuwa zinatolewa kwa mwaka huo zinakuwa tathmini za mwaka uliopita.

Bunge laahirisha kujadili muswada wa bima kwa wote

“Kwa maana hiyo hiki alichokisema Prof. Muhongo kwamba tumeshuka mwaka 2022, tathmini hiyo hata haijafanyika. Takwimu hiyo itatolewa Julai Mosi 2023 kwa maana hiyo zile takwimu walizozitoa sizo, na zile ambazo zimekwishatolewa mpaka sasa ambazo zinaongelea kwa mwaka uliopita zilizotolewa kwa mwaka huu zinaonyesha Tanzania bado tuko kwenye dola 1140 ambayo tumepiga hatua kubwa sana,” amesema Dkt. Mwigulu

Aidha ameeleza kuwa Benki ya Dunia imeandika ikionyesha kusikitishwa kutokana na taarifa iliyoandikwa kwenye tovuti moja ikisema Tanzania imeshuka kutoka uchumi wa kati kwenda kwenye uchumi wa chini na kwamba Benki hiyo imesahihisha kuwa bado Tanzania iko kwenye uchumi wa kati.

Dkt. Mwigulu amewahakikishia Watanzania kuwa Tanzania haitoshuka kwenda kipato cha chini badala yake inasonga mbele kuelekea kipato cha kati cha juu.

Send this to a friend