Serikali imesema hali ya ukosefu wa ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 nchini Tanzania imekuwa ikiongezeka kutoka asilimia 12.1 kwa mwaka 2014 hadi asilimia 12.6 kwa mwaka 2020/21.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya kwa mwaka wa Fedha 2023/24 bungeni jijini Dodoma.
Mwigulu amesema tatizo hilo la ajira ni kubwa zaidi nchini hasa kwa vijana wa kike wenye asilimia 16.7 ikiwa ni mara mbili ya kiwango kwa vijana wa kiume ambao wana asilimia 8.3.
“Tatizo hili ni la kihistoria tangu uhuru wa nchi yetu ambapo wakati tunapata uhuru tulikuwa na madaktari 12, wahandisi 2, tulikuwa na chuo kikuu kimoja kilichodahili wanafunzi 14, shule za sekondari zilikuwa 41 na wanafunzi 11,832, shule za msingi zilikuwa 3,270 na wanafunzi 486,470,” amesema.
Ameongeza “Tulipopata uhuru kazi ya kwanza ilikuwa ni kujenga sekta ya utumishi wa umma ambapo viongozi wote wa Serikali na wananchi wote walihamasisha watoto waende shule ili wawe watumishi wa Serikali. Kwa kipindi hicho, iliwezekana kuajiri wahitimu wote serikalini kwa nafasi ambayo muhitimu ataipendelea hata bila uwepo wa sekta binafsi.”