Mwili wa Askari wakutwa umetupwa msituni Zanzibar

0
78

Kufuatia upelelezi uliokuwa ukifanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja baada ya taarifa ya kupotea kwa Askari Haji Machano Muhamedi wa kikosi cha VALANTIA (KVZ) Makao Makuu Mtoni Zanzibar toka Agosti 8, 2024, Jeshi la Polisi limesema limepata mwili wake ukiwa umetupwa msituni.

Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi, imesema askari huyo alikuwa akihudhuria mafunzo ya Uongozi (Officer Cadet) katika Chuo cha Uongozi cha Jeshi la Kujenga Uchumi Dunga, ambapo majira ya saa 8 mchana katika msitu uliopo karibu na chuo hicho, askari huyo akiwa na wenzake katika mafunzo alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Septemba 26, 2024 majira ya saa 10 alasiri katika msitu huo, ulionekana mwili wa binadamu ukiwa umeharibika vibaya, na uchaguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ulibaini mwili huo ukiwa na nguo na viatu ambazo zinafanana na zile alizovaa askari huyo siku aliyopotea.

“Katika mfuko wa suruali aliyokuwa amevaa ilipatikana simu ambayo imetambulika kuwa ni ya kwake aliyokuwa akiitumia,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, Jeshi la Polisi limesema uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea ikiwemo ulinganisho wa vinasaba (DNA) kwa madhumuni ya kubaini ni kitu gani kilichomkuta na kupelekea kupoteza maisha ili hatua zaidi zichukuliwe.

Send this to a friend