Mwili wa Mchungaji wahifadhiwa mwaka mzima wakingojea afufuke

0
42

Mwili wa Mchungaji Siva Moodley mwanzilishi wa The Miracle Center kaskazini mwa Johannesburg nchini Afrika Kusini umesalia kwenye chumba cha kuhifadhi maiti kwa madai kuwa familia yake inafanya maombi ili afufuke.

Moodley alifariki Agosti 15, 2021 baada ya kuugua, huku familia yake ikificha juu ya kifo chake kwa waumini wa kanisa lake na kwenye mitandao ya kijamii.

Meneja katika nyumba aliyohifadhiwa Moodley, Martin du Toit amesema amewasilisha ombi katika Mahakama ya Johannesburg ili kumpa kibali cha mwili kuzikwa au kuchomwa moto, kutokana na familia yake kutofika kuutembelea tangu Septemba, mwaka jana.

“Baada ya kifo cha Mchungaji Moodley, familia yake na waumini wa kanisa hilo walikuwa wakitembelea msiba huo kwa ajili ya kumuombea afufuke. Ziara ya mwisho ilikuwa Septemba mwaka jana, hakuna mtu aliyekuja kuutazama mwili huo tangu wakati huo,” amesema Du Toit.

Inadaiwa, ibada katika kanisa hilo zimekuwa zikiendelea kama kawaida na zinaendeshwa na mkewe Jessie, mwanawe David, na bintiye Kathryn Jade. Huduma hizo pia zinaoneshwa moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii huku akaunti zake zikifanya kazi na jumbe zikitumwa kila siku kana kwamba zinatoka kwake.

Moja wa waumini wake amesema “kila tukiuliza yuko wapi huwa hatupati jibu, awali tuliambiwa anarudi muda si mrefu lakini mwaka umepita. Hakuna kitu, tumesoma taarifa za kifo chake kwenye vyombo vya habari na tunataka familia yake ifanye jambo sahihi na kumpa mazishi anayostahili.”

Send this to a friend