Mwili wa mwanafunzi wa tatu kati ya wanne wa Shule ya Msingi Kagera mkoani Kigoma waliofariki dunia baada ya mtumbwi uliokuwa umewabeba kuzama katika mto Ruiche, Manispaa ya Kigoma umepatikana leo.
Mwili huo uliopatikana ni wa mtoto Ashura Ramadhani (6), na kufanya idadi ya miili ya watoto hao waliopatikana kufikia mitatu, huku Vikosi vya Zimamoto na Uokoaji vikiendelea kuutafuta mwili wa mtoto mmoja uliosalia ambao haujapatikana mpaka sasa.
Aidha, Serikali kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia inatarajia kuanza ujenzi wa mradi wa barabara wa kilomita mbili pamoja na daraja katika eneo hilo ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Athuman Msabila amesema barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami na inatarajia kuanza mapema na kwamba hatua za awali zimeanza kufanyika.
Mnamo Februari 24 mwaka huu wanafunzi wanne kati ya sita walizama majira ya saa mbili asubuhi wakati wakivuka ng’ambo kuelekea shuleni. Watoto wawili kati ya sita waliokolewa wakiwa hai.