Mwongozo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi katika mwaka wa masomo 2019/2020
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020 unaotaja sifa, vigezo na utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mikopo ya elimu ya juu na kuwasihi waombaji mikopo watarajiwa kuusoma kwa makini na kuuzingatia.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amewaambia wanahabari leo (Jumanne, Juni 4, 2019) jijini Dar es salaam kuwa lengo la kutoa mwongozo huo ni kuwawezesha waombaji mikopo kuandaa nyaraka muhimu zinazotakiwa.
Kwa mujibu wa Badru, HESLB imetoa mwongozo huo kabla ya kufungua mfumo wa maombi ya mkopo ili kuwawezesha waombaji mikopo watarajiwa kuandaa nyaraka muhimu. Mfumo wa maombi kwa njia ya mtandao utafunguliwa Juni 15, 2019 na utafungwa Agosti 15, 2019.
Uzoefu na sababu za kutoa mwongozo
“Uzoefu wetu unaonesha kuwa waombaji wengi hukimbilia kwenye mtandao na kujaza fomu za maombi wakati mwingine bila kusoma mwongozo. Mwaka huu tumetoa mwongozo huu kwanza ili wausome kwa wiki takribani mbili kabla ya kuruhusiwa kuanza kujaza fomu kwa njia ya mtandao,” amesema Badru na kuongeza kuwa katika mwaka 2018/2019, waombaji zaidi ya 9,000 kati ya 57,539 waliokuwa na sifa za msingi walikosea kujaza fomu za maombi.
Ili kutatua tatizo hilo mwaka 2019/2020, Badru amesema HESLB imetembelea shule za sekondari 81 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar na kukutana na wanafunzi 27,489 ambao walielimishwa kuhusu sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa usahihi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema mwongozo huo unapatikana katika lugha za kiingereza na kiswahili katika tovuti ya HESLB ambayo ni www.heslb.go.tz
“Pamoja na mwongozo huo, pia tumeandaa kijitabu chenye maswali na majibu yanayoelekeza namna ya kuomba mkopo kwa lugha ya kiswahili … nacho pia kinapatikana kwenye tovuti yetu na tunawashauri wakisome,” amesema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Nyaraka muhimu za kuandaa
Waombaji wote wanatakiwa na vyeti vya kuzaliwa ambavyo vimethibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA). Aidha, kwa waombaji mikopo ambao wazazi wao wamefariki dunia, watatakiwa kuwa na nakala za vyeti vya vifo ambavyo vimethibitishwa na RITA au ZCSRA.
“Vilevile tunafahamu kuwa kuna wanafunzi waliofadhiliwa na taasisi mbalimbali katika masomo yao ya sekondari au stashahada, hawa wanatakiwa kuwa na barua kutoka katika taasisi hizo,” amesema Badru katika mkutano huo uliohudhuriwa na Mkurugenzi wa Upangaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronika Nyahende.
Kwa wanafunzi wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu, Badru amesema wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu wao kutoka kwa waganga wakuu wa wilaya au mikoa.
Maeneo muhimu yaliyoboreshwa kwa 2019/2020
Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo aligusia maeneo muhimu yaliyoboreshwa katika utoaji mikopo kwa lengo la kuwafikia wanafunzi wahitaji wengi zaidi.
“Baada ya kupokea maoni ya wadau, tumeongeza umri wa waombaji mikopo kutoka miaka 33 hadi 35 na pia mwaka huu tutapokea maombi kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita au stashahada ndani ya miaka mitano iliyopita … kabla ilikuwa miaka mitatu tu,” amesema Badru.
Malengo na bajeti
Katika mwaka wa masomo 2019/2020, Serikali kupitia HESLB imepanga kutoa mikopo na ruzuku ya elimu ya juu yenye thamani ya TZS 450 bilioni kwa jumla ya wanafunzi 128,285. Kati ya hao, wanafunzi 45,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza. Mwaka huu 2018/2019, unaoelekea mwisho; jumla ya TZS 427.5 bilioni zilitolewa kwa jumla ya wanafunzi 123,000.