Mzee Kiuno aweka rekodi ya kuongoza Uenyekiti wa Mtaa kwa miaka 30

0
5

Mwenyekiti wa mitaa mwenye umri wa miaka 70, Hamis Lukinga maarufu kama ‘Mzee Kiuno,’ ameendelea kuandika historia baada ya kuchaguliwa tena kuongoza Mtaa wa Makaburi A, Morogoro, katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni.

Ushindi huo unampa fursa ya kuendelea na uongozi wake kwa miaka mingine mitano, ikiwa ni kipindi chake cha sita mfululizo tangu kuingia madarakani mwaka 1994.

Lukinga, anayewakilisha Chama cha Mapinduzi (CCM), alichukua nafasi hiyo kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1994 na tangu wakati huo, ameendelea kushinda kwa kuaminiwa na chama pamoja na wakazi wa mtaa wake.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Mzee Kiuno ameeleza kuwa siri ya mafanikio yake ni kujitolea kwa dhati, uwazi, na uhusiano wake wa karibu na jamii huku akisisitiza kuwa maendeleo na mwongozo thabiti ni msingi wa uongozi wake, badala ya kutoa msaada wa kifedha.

“Kwenye mtaa huu, nimekuwa nikisaidia wakazi kwa mambo mbalimbali, si kwa pesa, bali kwa ushauri na kuwaelekeza hasa wanapokumbana na changamoto,” alisema Lukinga.

Wakazi wa Makaburi A wameonyesha furaha na kuridhishwa na uongozi wake, wakimtaja kama kiongozi mwenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo na mshikamano wa kijamii.

Send this to a friend