
Mahakama ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imemhukumu Fredy Samwel Kumigwa (60), mkulima na mkazi wa Mtaa wa Nyerere, Kumnyika Kasulu, kutumikia kifungo cha miaka 40 jela na kulipa fidia ya Shilingi milioni 1, kwa kosa la kumbaka msichana wa kazi za ndani mwenye umri wa miaka 15.
Tukio hilo limetokea Oktoba17, 2024 nyumbani kwa mshtakiwa wakati ambao hakukuwa na mtu mwingine nyumbani na baada ya tukio hilo, inadaiwa kuwa mhanga alifichwa na mtoto wa mshtakiwa aitwaye Mary Fredy, mkazi wa Kasulu, na kuagizwa asiseme chochote kuhusu tukio hilo.
Mshitakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 11, 2024 akituhumiwa kumbaka binti yake wa kazi za ndani.
Mahakama imeeleza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha uliothibitisha kwamba mshtakiwa alitenda kosa hilo, hivyo kutoa adhabu hiyo kama fundisho kwa wengine.