Mzee wa Upako ataka yeyote anayetaka kugombea awe na cheti na mafunzo ya JKT

0
64

Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Dar es Salaam, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako ameshauri kuwepo utaratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka kuhitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kama moja ya kigezo mwanasiasa kuruhusiwa kugombea nafasi ya uongozi nchini.

Akizungumza katika Kongamano la Viongozi wa Dini la kumtakia heri ya kuzaliwa na baraka za mwaka mpya Rais Samia Suluhu Hassan, kiongozi huyo amesema baadhi ya wanasiasa kutoifahamu nchi yao kwa kukosa uzalendo ndio sababu kubwa inayowafanya waidhihaki nchi mara kwa mara.

Lusekelo amesema kwamba Mwalimu Julius Nyerere alifanikiwa sana kuwaanda viongozi wazalendo kwa sababu ya mafunzo ya JKT, na kwamba kuondolewa kwa utaratibu huo kumesababisha ombwe.

“Sasa hivi wanasiasa wote hakuna mahali wanafundishwa historia ya nchi hii, siasa za nchi hii na mambo ya nchi hii. Mtu anatoka huko alikotoa, kadi ya chama, mbunge au diwani,” ameeleza Lusekelo akisema ni muhimu cheti za kufuzu mafunzo ya JKT nacho kiwe moja ya kigezo.

“JKT liwe suala la kitaifa, sio la chama. Wanakwenda kujifunza mambo ya nchi, miiko ya nchi. Sivyo, utakuwa na wanasiasa wa ajabu sana, wengine madiwani, wengine wabunge wa ajabu kabisa hawaijui nchi, mtu anakwenda Ulaya, mwingine Marekani anaitukana nchi yake,” amesisitiza.

Akizungumza katika Kongamano hilo lililojumuisha viongozi kutoka dini mbalimbali, Sheikh Musa Kundecha amesema Rais Samia ameonesha mfano wa matumizi mazuri ya muda kwa yale aliyoyafanya akiwa madarakani na kurejesha tumaini kwa Watanzania.

“Thamani ya maisha ya mwanadamu ni madhumuni ya kuwepo kwake, na sio muda anaoutumia kuishi hapa duniani. Mama Samia ametuonesha namna bora ya muda anavyoutumia kuwepo hapa dunia, karudisha matumaini ya Watanzania,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amepiga simu kwenye kongamano hilo na kuwashukuru viongozi wa dini kwa yale yote waliyoyasema, na akawaomba waendelee kumuombea na kuimarisha umoja wa kitaifa ili aweze kuliongoza vizuri kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Januari 27 mwaka huu Rais aliadhimisha kumbukizi ya kuzaliwa ambapo alitimiza umri wa miaka 62.

Send this to a friend