
Serikali ya Kaunti ya Nairobi inajiandaa kujenga soko la miraa (mirungi) katika eneo la Ziwani, Kaunti Ndogo ya Starehe, baada ya kupata idhini kutoka kwa wafanyabiashara wa eneo hilo kwenye mkutano wa kushirikisha wananchi.
Waziri wa Biashara na Fursa kwa Wajasiriamali, Dkt. Anastasia Nyalita, amesema kuwa ujenzi wa soko hilo ni moja ya vipaumbele vya utawala wa Gavana Sakaja ili kutoa mazingira bora kwa wafanyabiashara wa mirungi.
“Tumejipanga kujenga masoko 20 ya kisasa katika kaunti. Hadi sasa, tumekamilisha masoko manne; Karen, Mutuini, Kahawa West, na Juja, na hili litakuwa la tano. Baada ya ujenzi kukamilika, tutakuwa na mpango mzuri wa kugawa nafasi kwa wafanyabiashara,” amesema Dkt. Nyalita.
Afisa Mkuu wa Masoko na Biashara, Bi. Jane Wangùi, amethibitisha kuwa bajeti ya soko hilo tayari ipo na mipango yote imeshakamilika kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Uongozi wa eneo hilo umesema umekuwa ukipigania ujenzi wa soko la miraa kwa miaka kumi, na kwamba wanamshukuru Gavana kwa kupata bajeti inayohitajika kutimiza ndoto yao.