NALA yaungana na Vodacom M-Pesa kuleta namna rahisi ya kutuma na kupokea pesa katika nchi za Ulaya.

0
14

Kampuni ya Kimataifa ya NALA na kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kupitia M-Pesa wametangaza ushirikiano utakaowezesha watanzania walioko nchi za Umoja wa Ulaya (EU) kutuma na kupokea pesa kirahisi, haraka na kwa gharama nafuu.

Kampuni hizo mbili, zimeingia ushirika huo leo Januari 31, 2023 jijini Dar es Salaam zikiwa na lengo la kuhakikisha utumaji pesa unakuwa wa haraka, salama, wenye kuaminika na wenye gharama nafuu hapa nchini na kunaongeza matokeo chanya kwa kampuni za Kiafrica na kuzirahisishia mifumo yake ya malipo.

Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni (kushoto)na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya NALA, Benjamin Fernandes wakikabidhiana mkataba wa ushirikiano wa kibiashara wa kutuma na kupokea fedha kutoka nchi 19 za Ulaya wakatai wa hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makubaliano ya ushirikiano huo, Afisa Mtendaji Mkuu na Mwanzilishi mwenza wa NALA, Benjamin Fernandes amesema, kupitia huduma hiyo mtu aliyeko nje ya nchi anaweza kutuma pesa kwenda Tanzania kwa haraka zaidi kuliko kwenda kutuma kwa njia zingine.

Fernandes amesema, “nikiwa ni Mtanzania, ushirikiano huu unanipa furaha kuwafikia robo ya Waafrika wenzangu wanaoishi Ulaya kwa kuwapa huduma rahisi na ya kuaminika ya kutuma pesa nyumbani kwa kupitia Vodacom M-Pesa tunaiunganisha miundombinu na hivyo kuleta daraja la malipo kati ya nchi za Uingereza, Marekani na jumuiya ya Ulaya na Tanzania”, amesema

Amesema kupitia huduma hii Nala imezidi kuongeza wigo wake kijiografia kupitia bidhaa na kwa kuboresha miundombinu na hivyo kuendeleza nia yao ya kupeleka fursa za kiuchumi kwa waafrika pote duniani

“Mpaka sasa Nala, imetanua huduma zake katika bara la Ulaya kwa kuongeza nchi 19 zilizoko barani humo baada ya kuanza kutoa huduma katika nchi za Marekani ikitokea Uingereza” amesema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya NALA, Benjamin Fernandes, akionyesha jinsi ya kutuma na kupokea pesa kutoka nchi 19 za Ulaya kupitia M-Pesa, wakatai wa uzinduzi wa hafla hiyo jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni na Meneja Masoko wa M-Pesa, Noel Mazoya

Amesema, NALA ina nia ya kuiunganisha Dunia kwa kuwawezesha Waafrika wanaoishi nchi za Ulaya kutuma pesa Tanzania na nchi nyingine za Africa. Kwa kushirikiana na Vodacom M-Pesa, upanuzi huu unaongeza umuhimu wa kutuma na kupokea pesa kwa haraka na gharama rahisi kupitia huduma hii.

Amesema, licha ya kuwepo kwa mifumo mingi ya kutuma na kupokea pesa kuja Africa kutoka mabara mengine bado huduma zake ni za gharama sana hivyo kwa kulitambua hilo NALA imefanya juhudi kubadirisha namna ya utumaji wa pesa ili kuleta huduma rahisi na za wazi za kifedha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa M-Commerece, Epimack Mbeteni, ameupongeza ushirikiano huo huku akiongeza kwamba unaendana na mipango ya kampuni katika kukuza huduma ya utumaji pesa kimataifa (IMT) kwani wateja wa Vodacom M-Pesa sasa wanaweza kutuma na kupokea pesa kutoka nchi zaidi ya 200 moja kwa moja kwenda kwenye akaunti zao za M-Pesa.

“Tumetumia ubunifu na ushirikiano wetu ili kuhakikisha tunawezesha utumaji na upokeaji pesa kimataifa katika bara la Afrika na dunia kwa ujumla na hivyo kuiwezesha dunia kutuma pesa kirahisi zaidi na kuwezesha biashara kati ya mipaka ya nchi.

Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni (kushoto)na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya NALA, Benjamin Fernandes wakikabidhiana mkataba wa ushirikiano wa kibiashara wa kutuma na kupokea fedha kutoka nchi 19 za Ulaya wakatai wa hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Meneja Masoko wa M-Pesa, Noel Mazoya.

Amesema wanayofuraha kubwa kushirikiana na Nala, kampuni ambayo inatokea nchini Tanzania lakini inabadilisha namna na jinsi ya kutuma pesa duniani.

Ameongeza kuwa, ushirikiano huo utaambatana na kampeni itakayowazawadia wateja wa NALA na M-Pesa pindi watakapotumia huduma hii ambapo wateja wapya watazawadiwa na Nala kiasi cha dola 10 pindi watakapotuma kwa mara ya kwanza.

Pia kutakuwa na nafasi ya kujishindia tiketi mbili za ndege (kwenda na kurudi) kwa wateja watakaotuma pesa kwenda M-Pesa. Tiketi hizi zitatolewa kwa wateja watakaotuma au kupokea pesa kutoka nchi za Uingereza, Marekani, Jumuiya ya Ulaya (Austria, Ubelgiji, Cyprus, Estonia, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ugiriki, Ireland, Italia, Lithuania, Luxembourg, Malta, Uholanzi, Ureno, Slovakia, Slovenia, Hispania) katika kipindi cha mwezi Aprili kwa ajili ya Pasaka au Eid.

Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni (katikati) akizungumza na waandishi wa habarai Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wa kibiashara wa kutuma na kupokea fedha kutoka nchi 19 za Ulaya kupitia Kam puni ya NALA. Kulia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya NALA, Benjamin Fernandes na Meneja Masoko wa M-Pesa, Noel Mazoya.

Kwa nchi za Jumuiya ya Ulaya, NALA inapatikana kwenye App Store na Play Store kwa ajili ya kupakua.