Serikali ya Namibia imetangaza kupiga marufuku usafirishaji wa madini ya lithiamu ambayo hayajachakatwa na madini mengine muhimu.
Nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika ina akiba kubwa ya lithiamu, ambayo ni muhimu kwa hifadhi ya nishati mbadala, pamoja na madini adimu ya ardhini kama vile dysprosium na terbium zinazohitajika kwenye sumaku katika betri za magari ya umeme na mitambo ya upepo.
“Baraza la Mawaziri liliidhinisha marufuku ya usafirishaji wa baadhi ya madini muhimu kama vile madini ya lithiamu ambayo hayajachakatwa, kobalti, manganese, grafiti na madini adimu ya ardhi,” Wizara ya Habari ya Namibia imesema katika taarifa yake.
Hospitali ya Muhimbili yapiga marufuku mifuko ya plastiki
Ni kiasi kidogo tu cha madini kilichoainishwa kitaruhusiwa, baada ya kuidhinishwa na waziri wa madini, imeeleza zaidi taarifa hiyo.
Namibia ni moja ya wazalishaji wakubwa duniani wa madini ya uranium na almasi zenye ubora wa vito. Mwaka jana ilitia saini makubaliano ya kusambaza madini adimu kwa Umoja wa Ulaya chini ya mpango wa umoja huo wa kupunguza utegemezi wake kwa China kwa madini muhimu.