Namna bora ya kujitunza wakati wa ujauzito

0
43

Wakati wa ujauzito ni wakati ambao unahitaji kufanya vitu kwa uangalifu zaidi na kufuata taratibu zilizopendekezwa na wataalam, kwani makosa yoyote yanayofanyika yanaweza kumuweka mama mjamzito pamoja na mtoto kwenye hatari.

Kupitia mambo, haya yafuatayo yanaeleza namna bora za kujitunza wakati wa ujauzito na kuepuka madhara kwa mama na mtoto;

Kazi na mazoezi ya mwili
Mjamzito anaweza kuendelea kufanya kazi zake kama kawaida isipokuwa aepuke kuuchosha mwili. Anashauriwa kufanya kazi na mazoezi ya mwili kwa wastani kwa sababu humsaidia kuzuia kufunga choo, kupata usingizi mzuri, hamu ya kula na mzunguko wa damu kufanya kazi vizuri mwilini. Moja ya mazoezi mazuri kwa mjamzito ni kutembea asubuhi kabla jua halijawaka na wakati wa Magharibi.

Mapumziko
Mjamzito ni lazima apate usingizi wa kutosha usiopungua saa nane au tisa, ikiwezekana alale usingizi kwa muda mfupi mchana. Ikiwa hana mazoea ya kulala mchana basi ajitahidi kulala angalau nusu saa. Wakati wa kupumzika aketi akiwa amenyoosha miguu na ajilaze mahali panapofaa angalau kwa dakika 15.

Kupata choo
Ni vizuri mjamzito apate haja kubwa ipasavyo angalau mara moja kwa siku, hali kadhalika apate haja ndogo kama kawaida. Ni muhimu apate choo vizuri kwa sababu humsaidia kutoa masalio ya chakula yasiyohitajika mwilini. Kuharisha, kupata choo kigumu isivyo kawaida ni hatari, mjamzito akipata hali yoyote kati ya hizo ni lazima amwone daktari.

Mavazi
Mjamzito anatakiwa avae nguo zisizobana na zinazofaa kulingana na hali ya hewa. Nguo zisizobana humwezesha kupumua vizuri na kufanya shughuli zake bila shida. Anashauriwa kuepuka kufunga mkanda tumboni, avae sidiria inayoshikilia matiti vizuri ilimradi isiwe ya kubana. Asivae nguo za ndani zinazombana na avae viatu vinavyomsaidia kutembea bila tabu.

Mahangaiko
Mjamzito ajitahidi sana kuwa katika hali ya utulivu, hali ya hasira, ugomvi, kero huathiri afya yake. Kuvuta sigara au tumbaku kunaweza kuharakisha mapigo ya moyo ya mtoto na kuathiri afya ya mama na mtoto.

Kliniki za wajawazito
Mama akigundua ni mjamzito, aanze kliniki iliyo karibu naye mapema. Anapaswa kuendelea kwenda muda wote wa ujauzito.

Dawa
Mjamzito asijaribu kutumia dawa ambazo hazikupendekezwa au kuthibitishwa na daktari. Baadhi ya dawa ni hatari kwa mama na mtoto aliye tumboni, kwani huweza kusababisha kuharibika kwa mimba, kuzaa mtoto mwenye ubovu au mwenye hitilafu kadhaa kimwili na kiakili.

Send this to a friend