Siasa za Afrika zimechagizwa kwa kiasi kikubwa na mfungamano wa kifamilia na hii inadhihirika zaidi namna viongozi waliopo madarakani wanavyowaandaa watoto wao kwa namna moja au nyingine kurithi mikoba yao.
Zipo baadhi ya nchi tayari hili limeshadhihirika, wakati katika nchi nyingine inaonekana ndipo zinapoelekea.
Tutatupia jicho katika baadhi ya nchi za Afrika ambapo kwanza ni Congo-Brazzaville, ambapo Rais wa nchi hiyo Denis Sassou-Nguesso amemteua mwanae, Denis-Christel kuwa waziri.
Si jambo baya, lakini kitendo hicho kimeibua tetesi ambazo tayari zilikuwepo kuwa Rais huyo mwenye miaka 77 anamwandaa mwanae kupokea kujiti kutoka kwake.
Nchini Gabon Rais Ali Bongo Ondimba ni mtoto wa Omar Bongo ambaye aliongoza taifa hilo kuanzia 1967 hadi 2009.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haikuachwa nje ya hili ambapo Joseph Kabila alitwaa madaraka kufuatia kifo cha babaye, Laurent Kabila, ambaye aliuawa mwaka 2001. Joseph Kabila aliliongoza taifa hilo kwa miaka 17.
Nchini Equatorial Guinea, Rais Teodoro Obiang aliingia madaraka baada ya kumpindua mjomba wake, Francisco Macías Nguema mwaka 1979. Kama hiyo haitoshi, mwanae, Teodoro Nguema Obiang Mangue ndiye makamu wa Rais, nafasi ambayo inampa urahisi wa kumrithi babaye.
Kwingineko nchini Chad, baada ya Rais Idriss Déby kufariki dunia kutokana na majeraha aliyopata katika mapambano dhidi ya waasi, mwanae, Mahamat amejitangaza kuwa ndiye Rais wa serikali ya mpito.
Kama hiyo haitoshi, huko Afrika Magharibi, kuna tetesi kuwa Franck Biya anaandaliwa kumrithi babaye, Paul Biya (88) kama Rais wa Cameroon. Kwa muda mrefu Franck hayupo kwenye siasa, lakini kwa siku za hivi karibuni kumezuka kampeni zinazodaiwa ni wananchi wakimpigia chapuo kuwa anafaa kuwa kiongozi.
Afrika Mashariki nayo haikuachwa mbali kwani inadaiwa kuwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye sasa anaongoza kwa muhula wa sita (tangu 1986) anamwandaa mwanae, Jenerali Muhoozi Kainerugaba kurithi mikoba yake katika uchaguzi wa mwaka 2026.
Licha ya kuwa kwa nyakati nyingine watoto wa viongozi hawa hupatikana kwa njia ya kura, lakini endapo wanachaguliwa pale tu wazazi wao wanapotoka madaraka, hilo hutilia shaka uhalali wa kuchaguliwa kwao.
Suala la mtoto kuongoza nchi baada ya mzazi si tu lipo Afrika, limetokea maeneo mbalimbali ikiwamo Marekani (mara kadhaa), lakini suala kubwa la kuangazia ni namna watoto hao wanavyoingia madarakani.