Nape: Dkt. Slaa na wenzake wamekamtwa kwa tuhuma za uhaini, si vinginevyo

0
41

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hakuna mtu yeyote nchini ambaye amekamatwa au atakamatwa kwa kutoa maoni dhidi ya mkataba wa bandari au mradi mwingine wa Serikali na kubainisha kuwa watu watatu waliokamatwa walitoa vitisho vya kiuhalifu ikiwa ni pamoja na kuchochea kuipindua Serikali.

Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari kufuatia kukamatwa kwa Balozi Dkt. Slaa na wenzake, Waziri Nnauye amesema kukamatwa kwa watu hao kulikuwa kwa lengo la kutuma ujumbe kwa wahalifu ili kuwazuia kufanya makosa ya jinai na wala hakuingilii uhuru wa kutoa maoni nchini.

“Kukamatwa huko hakuwezi kwa njia yoyote kupunguza uhuru wa kutoa maoni nchini Tanzania, bali ni sehemu ya utekelezaji wa sheria, kuzuia machafuko ya kijamii yanayoweza kutokea kutokana na vitendo vya uhaini,” amesema.

Amesema tangu kuingia madarakani Machi 2021, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanua nafasi ya kidemokrasia na kiraia nchini Tanzania kwa kuondoa marufuku ya mikutano ya umma kwa vyama vya siasa, kuondoa marufuku ya magazeti kadhaa na televisheni za mtandaoni na kupanua uhuru wa kutoa maoni.

Aidha, ameongeza kuwa taarifa hizo zimechanganya mambo mawili tofauti ikiwa ni mjadala wa kitaifa kuhusu uwekezaji wa bandari unaoendelea nchini na suala la kuheshimu utawala wa sheria, hivyo “upotoshaji wa makusudi unaofanywa na vyombo vya habari kuhusu kukamatwa kwa washukiwa wa uhalifu unaweka shaka kuhusu nia na uaminifu wa mashirika yaliyotoa taarifa hizo.”

Waziri Nape amehitimisha kwa kusema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuheshimu uhuru wa kutoa maoni, kuruhusu mikutano ya amani na kuwezesha mjadala wa umma kuhusu masuala ya maendeleo ya kitaifa na mambo mengine ya maslahi ya umma na kuwahimiza Watanzania kuepuka matumizi ya lugha za hatari na uchochezi zinazohatarisha usalama wa taifa.

Send this to a friend