Nape: Haikuwa sahihi kuwalazimisha viongozi kununua laini za TTCL

0
41

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kwamba haukuwa utaratibu sahihi kuwalazimisha viongozi wa serikali kumiliki na kutumia laini za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Amesema kufanya hivyo kunaweza kusiwe na matunda yanayotarajiwa kwani kiongozi anaweza kuinunua kwa sababu amelazimishwa, lakini akatumia ya mtandao ambao yeye anaupenda.

“Huduma hizi hazilazimishwi. Ukiwalazimisha watu wachukue laini, watachukua hiyo uliyowalazimisha halafu watachukua na ile wanayoipenda,” amesema Nape na kuongeza kwamba “I don’t think if it was a good model [sidhani kama ulikuwa utaratibu mazuri.”

Nape amesema hayo akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari aliyetaka kujua wizara ina mpango gani kuhakikisha kwamba TTCL inafikisha mawasiliano vijijini ikizingatiwa kwamba Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza awatumishi wote wa serikali kuwa na laini za TTCL.

Aidha, katika mkutano huo wa kueleza mafanikio ya wizara kwa mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan iliibuliwa tena hoja ya gharama za intaneti na waziri akasema kwamba gharama zilivyo sasa zipo chini ya kiwango kinachokubalika kisheria.

“… kwa presha ya siasa tumeshuka hadi tukapitiliza kiwango kilichoiwekwa kisheria. Sasa hatuwezi kuendelea kushuka kama tunahitaji huduma bora,” amesema.

Amesema kuwa ukitaka huduma bora sharti ukubali kuigharamikia kidogo na kuwataka wananchi kuacha malalamiko, kujiona wanyongea au kudhani kwamba wanaonewa.

Hata hivyo, amesema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaendelea na mazungumzo na wadau kuona namna ya kuboresha gharama hizo ili kuimarisha na kukuza matumizi ya huduma za intaneti nchini.

 

Send this to a friend