Nape: Rasilimali za bara la Afrika zimegeuka laana

0
13

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka wanatasnia ya habari barani Afrika kuhakikisha wanaisaidia jamii kubadili mtazamo kwa kuona fursa zilizopo na kujivunia kuwa sehemu ya bara la Afrika lenye rasilimali za kutosha.

Waziri Nape amezungumza hayo akizindua maonesho ya utangulizi kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayofanyika Mei 3 ya kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu wa 2022 Tanzania imekuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kwa Bara la Afrika yanayofanyika jijini Arusha.

“Bara letu la Afrika lina rasilimali nyingi za kutosha na maeneo mengi rasilimali hizi zimegeuka kuwa laana kwa watu nadhani wakati umefika kwa wanahabari tuchukue uamuzi wa kusaidia bara letu lifaidike na rasilimali zake na watu wake waone matokeo ya baraka za rasilimali kwenye jamii zetu,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Inauma kuona tunateswa na rasilimali zetu wenyewe kwa sababu tunaona maeneo yenye rasilimali za kutosha ndio kwenye magomvi mengi na ndipo ambapo watu wake wanateseka sana lakini ukipewa hesabu ya rasilimali tulizonazo ukilinganisha na mabara mengine hatupaswi kuwa hapa tulipo, hivyo wanahabari tusimame kubadilisha mtazamo wa mambo haya na ninaamini inawezekana kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake.”

Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka huu wa 2022 yana kauli mbiu ya “Uandishi wa Habari na Changamoto za Kidijiti” kwa Bara la Afrika yanafanyika jijini Arusha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amethibitisha kuwa Mgeni Rasmi kwenye maadhimisho hayo.

Send this to a friend