Nape: Tutadhibiti usambazaji picha za ngono mitandaoni

0
73

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametoa tahadhari kwa watu wanaotumiwa picha za uchi kutozituma kwa watu wengine kwani kupitia TCRA ina uwezo wa kutambua nani amehusika kutuma picha hizo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu swali lililoulizwa na mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba juu ya hatua za Serikali kuzuia picha za ngono zilizoko mitandaoni ambazo amezitaja kuchochea udhalilishaji wa wanawake na watoto, Waziri Nape amesema Serikali imeongeza uwekezaji mkubwa huku ikiwa katika hatua za mwisho ili kudhibiti picha hizo.

LATRA: Tutawafungia madereva wa Uber na Bolt wanaofanya udanganyifu wa nauli

“Nilithibitishie bunge lako, tunao uwezo mpaka sasa wa kufuatilia na kujua nani anasambaza picha chafu, kwa hiyo nitoe tahadhari kwa watu ambao wanatumiwa picha, njia rahisi ukitumiwa picha chafu usiimtumie mtu, ni bora ukaifuta kwa sababu ukimtumia mtu mamlaka zina uwezo wa kujua nani kamtumia nani,” amefafanua Waziri Nape.

Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis amesema Serikali inaendelea kutoa elimu ya kuwalinda watoto wote dhidi ya ukatili, akiongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayegundulika kutuma picha za ngono katika mitandao ya kijamii.