Nauli za Uber na Bolt kupanda

0
45

Wakati madereva wa huduma za Bolt na Uber wakiomba LATRA kupandisha bei za nauli ili iwasaidie kufanya kazi kwa faida, wadau wa sekta ya usafiri wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia ili kuleta unafuu kwa wananchi kutokana na gharama za usafiri zinazotarajiwa kupanda.

Kulingana na mapitio ya nauli yanayoaminika kufanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) ambazo bado hazijatumika, zinatarajiwa kuongezeka kutoka 450 kwa kilometa hadi 900.

“Ni ngumu. Unampeleka mtu ana kulipa TZS 3,000 na umetumia lita moja ya mafuta ambayo ni TZS 2,630, na wakati huo unalipa asilimia 15 ya wenye mtandao,” amesema Samson John, dereva wa Uber.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe amesema wamefanya marekebisho hayo kwenye nauli za usafiri ili kuwawezesha madereva na makondakta kutekeleza shughuli zao kwa faida.

“Uwepo wa watoa huduma hizo umefanya upatikanaji wa usafiri kuwa rahisi na nafuu kwa wananchi, huku wakizalisha maelfu ya ajira kwa madereva wanaofanya kazi hizo,” amesema.

Akizungumza Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk. Abel Kinyondo alisema kuwa mafuta yamepanda kwa asilimia 13 na ili wafanyabiashara wapate faida wanapandisha bei pia, hii inamuathiri hata ambaye hana gari na athari yake itaendelea kusababisha ongezeko la mfumuko wa bei.

Aidha, Mwenyekiti wa Chakua, Hassan Mchanjama aliongeza kuwa ni vizuri Serikali kufuatilia mchakato huo na kudhibiti bei isipande zaidi ili kuwalinda wananchi maana wakiachwa wafanyabiashara wataangalia maslahi yao na kuwapa kisogo wananchi.

“Tunatoa agizo kwa Serikali, suala hili wanatakiwa kuwa makini, tunajua mafuta yamepanda lakini iwe makini kuangalia bei zake zisipande, wananchi wengi vipato vyao ni vya chini,” aliongeza.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend